Ndoto kuhusu Mvua   

Maana ya kuota kuhusu mvua hutegemeana sana na ukubwa wa mvua hiyo na urefu wa kipindi cha kunyesha kwa mvua hiyo. Mvua ya kawaida inaweza kuashiria kwamba kuna jambo linalokujia – linaweza kuwa zawadi, lakini linaweza pia kuwa jambo baya kama ugonjwa. Dhoruba inaweza kuashiria matatizo ama ugonjwa siku zako za mbeleni, na kwamba unaweza kukutana na udanganyifu ama huzuni maishani mwako. Lakini kama ukichukua hatua sahihi, bado unaweza kupata ushindi mwishoni. Kama ukiota kwamba mvua imekatika na jua limetoka, ndoto hii inaweza kuashiria kuja kwa bahati njema siku zako za mbeleni.

Wengine huamini kwamba mvua huashiria baraka katika ndoto. Hivyo mtu anapoota mvua inanyesha, basi afahamu kwamba kuna baraka na riziki zinazomjia maishani mwake.

Ukiota unanyeshewa na mvua, basi ndoto hii huashiria kwamba unasafishwa na kuondolewa masaibu yote yalikuwa yakikunzinga maishani mwako.

Ukiota kwamba kuna mvua kubwa na maji ya mvua hiyo yameingia nyumbani mwako, ndoto hiyo huashiria kwamba baraka na neema kubwa imekujia. Lakini kama mvua hiyo imeambatana na upepo mkali na dhoruba, basi ndoto hiyo hutafsiriwa kwamba misukosuko na balaa iko njiani kukupata na hivyo unapaswa kutafuta msaada wa kiroho ili uweze kuiepuka misukosuko hiyo.

Ukiota mvua inanyesha kwa jirani yako, lakini hainyeshi kwako, ndoto hii hutafsiriwa kwamba kuna mtu amekuroga ama anakufanyia vitendo vya kichawi.

Ukiota kwamba, mvua inanyesha lakini badala ya kuona maji ukawa unaona damu, basi ndoto hiyo hutafsiriwa kumaanisha kwamba kuna roho ya mauti inayokufuatilia wewe au inayofuatilia mtu wako wa karibu.

Ukiota upo safarini na mara mvua kubwa ikaanza kunyesha, nanyi watu ama chombo chenu cha usafiri kikakwama njiani, ndoto hii huashiria kwamba utapitia masaibu  au huzuni fulani katika safari yako ya maisha itakayokufanya ukwame na kushindwa kusonga mbele.

Leave a Reply