Kama ukiota kuhusu mbwa, ndoto hii inaweza kuashiria jambo jema ikiwa kama mbwa huyo ana tabia njema na anakutii, hasa mbwa mtoto. Hata hivyo, kama mbwa huyo anaonyesha tabia mbaya, anapigana ama anavunjavunja vitu, ndoto hii inaweza kuashiria kwamba utaingia matatizoni hivi karibuni hasa kutokana na watu wasio waaminifu. Kama mbwa huyo akikung’ata, basi kunaweza kuwa kuna mtu anayekupangia njama au hata kukuroga. Kama mbwa huyo anakubwekea ama kukungurumia, ndoto hii inaweza kuashiria maradhi au kifo kwenye familia yako. Kama ukiota kwamba mke mpya ameingia kwenye boma na mbwa wa boma hilo wamempenda badala ya kutaka kumng’ata, ndoto hii inaweza kuashiria kwamba mwanamke huyo amekubaliwa na mababu wa boma hilo.
Kama ukiota mbwa na vitoto vya mbwa, basi ndoto hii huashiria uwepo wa uzazi mzuri kwenye maisha yako au familia yako. Watoto wa mbwa kwenye ndoto huashiria furaha na amani katika maisha ya mtu.
Ikiwa utaona unafuatana na mbwa kwenye ndoto, basi ndoto hiyo huashiria ulinzi kwenye maisha yako. Hii inaweza kuwa kwamba kuna mtu fulani anayekulinda pasipo wewe kujua, ama kuna mtu fulani maishani mwako unayemlinda.
Wengine huamini kwamba ndoto zinazohusu mbwa huashiria nguvu za giza na hususani roho ya umalaya. Mtu anapoota kwamba ameng’atwa na mbwa, basi kuna wanaoamini kuwa mtu huyo atakuwa amerushiwa roho ya umalaya kwenye maisha au kizazi chake.