Ndoto kuhusu kurogwa / uchawi

Kama mtu, kama vile mchawi, akikuroga, inaweza kuwa kwamba anakuonea wivu wewe na kukionea wivu kile ulichonacho maishani mwako, na kwamba anataka jambo baya likupate, kama vile ajali au kifo.

Wengi huamini kwamba, ukiota kuwa kuna mtu anafanya uchawi dhidi yako au dhidi ya mtu mwingine, basi ndoto hii huashiria kwamba unajaribu kuonyeshwa kwamba kuna vitendo vya uchawi vinavyokuzunguka wewe ama vinavyozunguka familia yako. Mtu yule unayemwona kwenye ndoto akifanya uchawi, mara nyingi huwa si ndiye aliye mchawi kiuhalisia. Ni imani ya wengi kwamba, kwenye ndoto wachawi hujivika sura za watu wengine ili usiwatambue, ama ili kukuchonganisha wewe na mtu husika. Kwa mfano, unaweza kuota rafiki yako wa kike wa karibu anamroga mume wako. Ndoto hii inaweza kukufanya ukaanza kumhisi rafiki yako vibaya, kumchukia au hata kuvunja kabisa mahusiano yako ya kirafiki na yeye. Hili likitokea, basi jua kuna uwezekano mkubwa kwamba kuna mtu alikujia kwenye ndoto hii, akijivika sura ya rafiki yako, ili kusababisha mafarakano hayo kwenye mahusiano yenu. Hivyo basi, ndoto zinazohusu urogaji ama uchawi hazina budi kutafsiriwa kwa umakini na utulivu. 

Wengine huota ndoto za kichawi pale mabibi/mababu zao wanapojaribu kuwarithisha vikoba vya uchawi. Katika ndoto za namna hii, mtu anaweza kumwona babu/bibi yake aliyekwishafariki akifanya uchawi nyumbani/chumbani mwake. Na wakati mwingine hata kuona bibi/babu huyo akimuelekeza au kumfundisha kuhusiana na uchawi huo!

Hata hivyo, kuna ambao huamini kwamba huonyeshwa pale mtu fulani anapofanya uchawi dhidi yao au dhidi ya watu wao wa karibu. Kupitia maombi, kwa wale wanaomwamini Mungu, wao huamini kwamba wanaweza kuonyeshwa waziwazi ni nani anayewaroga ama kuwafanyia uchawi. Katika hali hii, mtu anapomwona mtu fulani akifanya uchawi dhidi yake au dhidi ya mtu wake wa karibu kwenye ndoto, basi mtu huyo huamini moja kwa moja kwamba mtu huyo aliyemwona kwenye ndoto akifanya uchawi ni mchawi kweli-kweli. Ikiwa muotaji huyo ataona kuwa anapigana na mchawi huyo kwenye ndoto na kumshinda, basi hilo hutafsiriwa kwamba mtu huyo amemshinda adui wake aliyekuwa akimfanyia vitendo vya kichawi na hivyo uchawi huo hautaweza tena kufanya kazi.

Pia, kuna wanaoamini kwamba mwanamke ambaye hajaolewa akiota kwamba kuna kijana anafanya uchawi au anamroga, basi ndoto hii inaweza kumaanisha kwamba mwanamke huyo ataingia kwenye penzi zito siku za hivi karibuni. Lakini kama teyari mwanamke huyo ameshaolewa, ndoto hiyo huweza kumaanisha kwamba kutatokea usaliti mkubwa katika ndoa ya mwanamke huyo.

Wengine huamini kwamba, ukiota kwamba nguo yako fulani ya ndani imeibiwa, basi ndoto hiyo huashiria kwamba kuna mtu wa karibu yako anayekuroga ama anayekufanyia uchawi.

Kunaswa kwenye Mtego na Kutishiwa

Kuna mtu anaweza kuwa anakuroga ikiwa kama utaota kwamba kuna mtu analiita jina lako kwenye korido ama kwenye eneo la ngazi. Na kisha wewe ukimfuata, unamuona kuwa amebeba kitu, kisha mnaanza kupigana hadi nyote mnaanguka chini, unapojaribu kutoka kwenye nyumba hiyo anakuwahi na kufunga mlango. Kisha unapopata njia ya kutoka nje, mtu huyo anakunyooshea kidole na kukuambia kuwa siku moja atakukamata. Mtu huyo anaweza kuwa anajaribu kukuroga ili akujeruhi, hata ikiwa kama mtu huyo ni ndugu au rafiki.

Mtoto Anayejinyea

Kama ukiota kwamba umebeba mtoto wako mwenye umri wa kama miaka mitano, naye akakunyea, kunaweza kuwa na mtu anayekuroga kwa kutumia nguvu za giza. Kinyesi cha mtoto wako ndotoni kamwe hakipaswi kukugusa kwa kuwa mtoto unayemuona ndotoni si mtoto wako.

Kulala na Mtu

Kama ukiota kwamba umelala na mtu, kisha ukaona kuwa kila mtu anakuchukia na pindi unapocheka kila mtu anakereka, ndoto hii inaweza kuashiria kuwa umerogwa.

Mawe na Vilima

Kama ukiota kwamba kuna mtu anakurushia mawe na kukukimbiza huku akiwa ameshikilia mawe, ndoto hii ni nzuri ikiwa kama utaweza kuyakwepa mawe hayo na kuamka kabla mawe hayo hayajakupata. Hata hivyo, ndoto hii inaweza kuashiria hatari kama moja au zaidi ya mawe hayo yatakupata, kwani hilo humaanisha kuwa kuna mtu ameweza kukuroga kwa kutumia uchawi wa jiwe, kwa kuzungumza na jiwe. Usiku yeye huliamuru jiwe hilo kuja kukupiga. 

Kama ukiota kama kuna mtu amekuning’iniza kwenye kilima cheusi ndoto hii inaweza kuashiria kuwa mtu huyo anataka kukudhuru, kukujeruhi ama kukuuwa. Katika hili unapaswa kwenda na kutafuta msaada kutoka kwa mganga wa kienyeji kwani siku moja mtu atakuachilia kutoka kwenye kilima hicho ili uanguke.

Leave a Reply