Kuota kuhusu Watu Waliofariki 

Ukiona watu waliokwishafariki kwenye ndoto, jambo hili kwa kawaida huwa si jambo zuri kwako. Kama watu hao wamerudi kwenye ulimwengu wa walio hai, ndoto hii inaweza kumaanisha kwamba kuna jambo baya lililo njiani kukujia. Kama watu hao ni ndugu zako, basi ndoto hiyo inaweza kumaanisha kwamba unapaswa kuacha kufanya mambo maovu, la sivyo utaingia matatizoni.

Kama ukiota kuhusu ndugu zako waliokwishafariki, ndoto hiyo huashiria kwamba ndugu zako hao wanataka kupitisha ujumbe fulani kwenda kwa watu walio hai. Wakati mwingine unaweza kuota kwamba ndugu hao wanalalamika kwamba wanahisi njaa. Ndoto kama hiyo humaanisha kwamba tafrija inapaswa kufanyika, ambapo mbuzi, ng’ombe au kuku watapaswa kuchinjwa, kwa ajili ya wao kula.

Ukimwota mtu ambaye amekwishafariki, mtu huyo akawa anakuangalia tu bila kukusemesha chochote, basi ndoto hiyo humaanisha kwamba kivuli cha mtu huyo hakina shida na wewe na kimekugeukia tu ili kuja kukutembelea au kuwa karibu na wewe. Hata hivyo, ikiwa mtu huyo aliyekwishafariki akikusemesha katika ndoto hiyo, basi jambo hilo hutafsiriwa kama roho ya mtu huyo imekuja kwako na inataka ikuchukue ili ukaishi nayo huko ilipo, hivyo mtu aliyeota ndoto hiyo anaweza kufariki ikiwa kama hatachukua hatua ya kupingana na matakwa hayo.

Wengine huamini kwamba, kama ukiota unamwona mtu ambaye amekwishafariki, basi ndoto hiyo hubeba roho ya mauti inayokufuatilia. Hii ndoto hulenga kukuunganisha na watu waliokwishafariki na hivyo kukuvuta katika ulimwengu wao na kukufanya ufanane na walio wafu.

Leave a Reply